RAIS Jakaya Kikwete jana alikuwa miongoni mwa marais walioshuhudia Felipe Nyusi akiapishwa kuwa Rais wa Tano wa Msumbiji. Nyusi aliapish...
Nyusi aliapishwa kwa kula kiapo cha kulitumikia taifa hilo mbele ya
Mwenyekiti wa Baraza la Katiba, Heremegildo Gamito, mbele ya umati wa
viongozi wa mataifa mbalimbali na wananchi wa Msumbiji.
Sherehe hizo zilipambwa kwa shamrashamra mbalimbali ikiwa ni pamoja
na burudani za kwaya, halaiki na gwaride rasmi, lililoandaliwa kwa ajili
ya Rais huku baadhi ya makundi ya wananchi wakiwa na fulana zenye
maneno ya Frelimo na picha za Rais Nyusi wakiimba na kucheza pembeni.
Mara baada ya kuapa, Rais Nyusi alitia saini kitabu maalumu, kisha
alikabidhiwa bendera na vitendea kazi, ambavyo aliwaonesha wananchi na
wageni waliohudhuria kuashiria kuwa amekabidhiwa rasmi nchi.
Rais Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi kutoka nchi za Jumuiya ya
Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na wanaotoka katika nchi
zinazozungumza Kireno, waliohudhuria sherehe hizo.
Ujumbe kutoka Tanzania pia uliwakilishwa na Rais mstaafu wa awamu ya
tatu Benjamin Mkapa, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim,
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed.
Mbali na viongozi wa Tanzania, wengine ni kutoka nchi za Swaziland,
Afrika Kusini, Malawi, Zambia, Lesotho, Zimbabwe na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Rais Nyusi ameingia madarakani akimrithi Rais Armando Guebuza baada
ya kujinyakulia kura kwa asilimia 57 na kumwangusha mpinzani wake na
Kiongozi wa chama cha Renamo, Alfonso Dhlakama aliyepata kura asilimia
36.6 katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 15 mwaka jana.
Hata hivyo, pamoja na ushindi huo, Rais Nyusi amepata asilimia chache
za kura ukilinganisha na wakati wa Rais Guebuza kwenye uchaguzi wa
mwaka 2009, ambapo alipata asilimia 75.
COMMENTS