Tanzania Sh. VS U.S Dollar Dar es Salaam. Wasomi...
VS
U.S Dollar |
Dar es Salaam. Wasomi nchini wamezungumzia kuhusu kupanda kwa thamani ya Dola ya Marekani dhidi ya Shilingi ya Tanzania na kusema kunasababishwa na kuongezeka kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kusababisha fedha nyingi kutafutwa ili kulipia bidhaa hizo.
Bidhaa hizo ambazo huingizwa nchini hulipiwa kwa dola, hivyo ukusanyaji fedha nyingi huhitajika ili kukidhi bei zinazoelekezwa na wafanyabiashara wa nje. Hii husababisha kuwa na uhitaji mkubwa wa dola kuliko shilingi.
Thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani jana iliuzwa kwa Sh1,813 katika maduka ya kubadilishia fedha. Hata hivyo kwa viwango vya Benki Kuu (BoT), dola iliuzwa kwa Sh1,768.
Mkuu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Profesa Winieaster Andasom alisema taifa linakabiliwa na tatizo kubwa la uagizaji bidhaa nyingi kutoka nje kuliko zile zinazouzwa nje.
Alisema ili uchumi wa taifa ukue na thamani ya shilingi iwe na nguvu, lazima Watanzania waongeze uwezo wa kuuza bidhaa zao nje na kwa fedha za kigeni. Aliongeza kuwa kitendo cha uagizaji bidhaa kwa wingi kutoka nje kinafanya matumizi ya shilingi kudidimia na kupoteza thamani.
Aliitaka Serikali kuagiza bidhaa muhimu tu kama mashine, mafuta na zana ambazo hazizalishwi nchini. Lakini bidhaa nyingine kama mazao ya chakula na sukari, alisema hamna haja ya kuagiza kutoka nje. Profesa Andasom pia alibainisha kuwa thamani ya shilingi inaporomoka, kutokana na mfumuko mkubwa wa bei.
Alisema wananchi ndiyo waathirika wakubwa kunapotokea na mfumuko wa bei na maovu mengi huongezeka katika jamii.
Naye Profesa Humphrey Moshi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisisitiza kuwa uagizaji wa bidhaa nje ya nchi kuliko zinazozalishwa nchini kunayanufaisha mataifa mengine kwa sababu wanauza kwa thamani ya fedha yao.
Profesa Moshi aliongeza kuwa njia pekee ya kutatua tatizo hilo ni kuweka mikakati ya kuboresha kilimo ili mazao mengi yauzwe nje. Alisema ni muhimu kuwa na kilimo kisichotegemea mvua, badala yake kuwe na kilimo cha umwagiliaji.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya alikiri kupanda kwa Dola ya Kimarekani na kusema kuwa, “hili liko wazi kwamba bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi ni nyingi kuliko zinazozalishwa nchini kwenda nje ya nchi.”
Aliongeza: “Kinachotakiwa ili dola isiendelee kupaa ni kuhakikisha tunazalisha bidhaa zenye ubora ili ziende kwa wingi nje ya nchi na hapo tutaweza kupambana na kupanda kwa dola.”
COMMENTS