MAKOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm na Charles Boniface Mkwasa wamesema hawana tatizo na kuikabili Etoile du Sahel ya Tunisia katika...
MAKOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm na Charles Boniface Mkwasa wamesema hawana tatizo na kuikabili Etoile du Sahel ya Tunisia katika raundi ijayo ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga ilisonga mbele katika raundi ya kwanza juzi licha ya kufungwa bao 1-0 na FC Platinum ya Zimbabwe katika mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Mandava mjini Zvishavane, kilometa chache kutoka mji wa Bulawayo.
Kwa matokeo hayo, Yanga ilisonga mbele kwa jumla ya mabao 5-2 baada ya kushinda mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa mabao 5-1, na sasa itakutana na miamba ya Tunisia, Etoile du Sahel.
Watunisia hao wamesonga mbele baada ya jana kutoka sare na Benifica de Luanda ya Angola ya bao 1-1 katika mechi ya marudiano iliyofanyika kwenye mji wa Luanda. Ilishinda mechi ya kwanza bao 1-0 mjini Sahel, hivyo kufuzu kwa jumla ya mabao 2-1.
Katika mechi nyingine za Kombe la Shirikisho zilizochezwa jana, Warri ya Nigeria ilisonga mbele kwa jumla ya mabao 2-0 baada ya sare ya 0-0 na Dedebit ya Ethiopia jana mjini Addis Ababa.
Rayon Sports ya Rwanda ilitolewa na Zamalek kwa jumla ya mabao 6-1 baada ya jana kufungwa mabao 3-0 mjini Kigali, Ferroviario Beira ya Msumbiji iilishinda Vita Cluba ya DRC, lakini ikatolewa kwa jumla ya mabao 3-1 na Clun African ya Tunisia iliitoa Dolphins ya Nigeria kwa jumla ya mabao 6-0, jana ikishinda 3-0 ugenini.
Katika mahojiano na gazeti hili jana alasiri wakiwa wanatazama mechi ya Benifica na Etoile, Pluijm na Mkwasa, wote walieleza kuwa miamba hiyo ya Tunisia ni wepesi kwa maana kuwa wanacheza mpira wa kiufundi zaidi, usio wa kasi na usio wa kutumia nguvu, hivyo ni wapinzani bora kulinganisha na Waangola.
“Kila mechi tutaikabili kwa mtazamo wake. Lakini kwa timu hizi mbili (Benifica na Etoile), Etoile ni nyepesi kwa sababu wanacheza tactical (kiufundi) siyo physical (kwa nguvu). Ni wazuri kucheza nao,” alisema Mkwasa.
Kocha wake mkuu, Pluijm aliunga mkono kauli hiyo akisema: “Kwa Tunisia ni wazuri, wanacheza sana kiufundi siyo physical na hawatumii kasi sana.”
Yanga itaikabili Etoile du Sahel kati ya Aprili 17 na 18, mwaka huu na marudiano kati ya Mei 1, 2 na 3, mwaka huu. Katika raundi ya awali, Yanga iliitoa BDF ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-2.
Mkwasa akizungumzia mechi ya juzi ya FC Platinum, alisema kipindi cha kwanza waliona tatizo katika sehemu ya kiungo na ndio maana kipindi cha pili kilipoanza walifanya mabadiliko ya kumwingiza Kelvin Yondani na kumtoa kiungo Said Juma ‘Makapu’, hali iliyoifanya Yanga icheze vizuri zaidi.
Aidha, Pluijm alisema wataendelea na programu zao za mazoezi kwa kutumia mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
“Hatuhitaji kuwa na mechi za kimataifa kwa sababu tuna mechi nyingi za Ligi Kuu, tutaendelea na programu zetu kwa kutumia mechi hizo,” alieleza Pluijm ambaye kikosi chake kilitua Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana na wachezaji kupewa mapumziko hadi leo watakapoendelea na mazoezi.
Timu hiyo inayoongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 40, itacheza na Coastal Union keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa.
COMMENTS