Last Updated on 17 January 2015 By Anna Makange, Tanga Hits: 63 Kaman...
- Last Updated on 17 January 2015
- By Anna Makange, Tanga
- Hits: 63
WAKAZI watano wa kitongoji cha Mafuriko Amboni kilichopo jijini Tanga
wamejeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili baada ya kurushiwa bomu
la kutupwa kwa mkono na mtu asiyejulikana wakati walipokuwa wakitazama
mpira kwenye banda la wazi.
Majeruhi hao ni Hassani Abdallah (72) ambaye amevunjika mguu wa kulia
na kupata madhara makubwa kifuani na sasa amelazwa katika hospitali ya
mkoa ya Bombo.
Wengine ni Rashid Ally (45), Mrisho Abdi (29), Juma Mtoo (15) na
Abdul Ismail (19) ambao waliumia sehemu mbalimbali za mwili lakini baada
ya kufikishwa Bombo wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Frasser Kashai amethibitisha tukio
hilo na kusema limetokea Januari 15 mwaka huu saa 3:00 usiku huko
Mafuriko wakati waathirika hao walipokuwa ndani ya banda moja la
kuonesha video.
“Ni kweli jana usiku huko Amboni Mafuriko katika kata ya Chumbageni
kulitokea mlipuko wa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu”, alisema.
Aidha aliongeza, “Bomu hilo lilirushwa majira ya saa 3:00 usiku
kwenye banda la wazi la kuonyesha video ambalo ni mali ya Evarist
Kingazi (82) na kusababisha majeruhi watano”, alisema.
Alisema uchunguzi wao wa awali umebaini kwamba bomu hilo ni la
kutengenezwa kienyeji kwa sababu askari waliofika eneo la tukio
walifanikiwa kuokota mabaki yake ambayo yamejumuisha vipande kadhaa vya
nondo na vibati vidogo vidogo.
Kamanda Kashai alisema mkazi mmoja wa eneo hilo, Ally Rashid (25)
anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano maalumu kuhusiana na tukio hilo.
COMMENTS