WANANCHI wa Kata ya Migombani, Jimbo la Segerea Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, jana walimwapisha Japhet Kembo wa Chama cha Demokr...
Sambamba na hilo pia wananchi hao waliwaapisha wajumbe watano wa kamati
ya mtaa huo, ambao ni Rose Mhagama, Flora Nyangeta, Angelo Machunda,
Paulina Mbalale pamoja na Ramadhan Rashid Seif wote Chadema.
Hatua ya wananchi hao imekuja baada ya mgombea huyo kushindwa
kuapishwa kuwa mwenyekiti halali wa mtaa huo katika shughuli za jumla za
uapishaji zilizofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Ilala hivi karibuni.
Wakizungumza na MTANZANIA katika eneo la Ofisi ya Katibu Mtendaji wa
Mtaa wa Migombani, baadhi ya wananchi kutekeleza azma hiyo walisema
wamekuwa wakipata shida kushughulikiwa matatizo yao kutokana na mtaa wao
kutokuwa na mwenyekiti kwa muda mrefu.
“Sasa hivi mtu kama una tatizo la kutatuliwa na mwenyekiti unaambiwa
hamna huduma kwani hawa watendaji wanadai si jukumu lao, kwa hiyo
tumeona ni bora kumwapisha mtu tuliyemchagua wenyewe ili kutuongoza na
tunaomba halmashauri iyatambue maamuzi haya vinginevyo vurugu
zitatawala,”alisema Gango Boniventure mkazi wa mtaa huo.
Diwani wa kata hiyo, Azuri Mwambagi (CHADEMA), alisema awali shughuli
hiyo ilipaswa kufanywa na mkurugenzi wa wilaya hiyo, lakini
ilishindikana kutokana na sababu zisizojulikana.
Alisema katika uchaguzi wa kwanza wa serikali za mtaa uliofanyika
Desemba 14 mwaka jana mgombea huyo alishinda kwa kura 547 dhidi ya kura
273 za mgombea wa CCM na 205 NCCR Mageuzi, lakini halmashauri ilishindwa
kumtangaza kwa shinikizo la mmoja wa viongozi wa juu wa serikali ambao
hawataki kuongozwa na wapinzani.
“Wananchi wa kata ya migombani tumeamua kumwapisha rasmi mgombea wetu
kwani matokeo ya uchaguzi yapo wazi na hata mkurugenzi alishakiri mbele
yetu kuwa Chadema ndo washindi katika jimbo hili lakini kutokana na
ubabe wa baadhi ya viongozi ambao wanafahamika wazi mkurugenzi amegoma
kumtangaza hadi sasa.
“Kwa hiyo kama kiongozi yeyote anataka vurugu na wananchi basi
ajaribu kutengua matokeo haya, kwa kuwa hili jambo limetendeka kihalali
kabisa, kwani hata sheria na kanuni za uchaguzi za serikali za mitaa
zinaeleza kuwa mshindi anapaswa kuapishwa na mkurugenzi wa manispaa,
makamishna wa viapo (wakili au hakimu),”alisema Mwambagi.
Mwenyekiti wa Chadema wa kata hiyo, Gango Kidera, alisema kwa mujibu
wa sheria za chama hicho, wanachama wanahaki na wajibu wa kumwapisha
kiongozi wao katika eneo walilomchagua.
Kwa upande wake Idd Msawanga, ambaye ni wakili wa kujitegemea
aliyemwapisha mwenyekiti huyo, alisema kuwa tendo hilo si kosa kisheria
kwani matokeo ya uchaguzi yapo wazi na halmashauri inayatambua.
Alisema endapo halmashauri isingeyatambua matokeo hayo, basi upinzani walipaswa kuweka pingamizi mahakamani baada ya uchaguzi.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Segerea, Justin
Nyangwe alisema hana taarifa za kuapishwa kwa mwenyekiti huyo pamoja na
wajumbe wake kwani halmashauri haikuwapa barua yoyote ya kumtaarifu.
Alisema ofisi yake haiwezi kumpokea na kufanya kazi na mwenyekiti
huyo kwani haimtambui na jukumu hilo hufanywa na halmashauri pekee
kupitia wanasheria na mawakili wake wanaotambulika.
Siku chache zilizopita mkurugenzi wa Wilaya ya Ilala alisema
hakuwaapisha washindi wa Migombani kutokana na kuwepo shinikizo kutoka
ngazi ya juu.
COMMENTS