Wachezaji wa Mtibwa Sugar wakishangilia ushindi Na Mwandishi Wetu, Zanzibar MABINGWA wa zamani wa Tanzania mara mbili mfululizo, ...
Wachezaji wa Mtibwa Sugar wakishangilia ushindi
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MABINGWA wa zamani wa Tanzania
mara mbili mfululizo, 1999 na 2000, Mtibwa Sugar ya Morogoro wametinga
fainali ya michuano ya Mapinduzi mwaka 2015 kufuatia kuitandika JKU ya
Zanzibar penalti 4-3.
Mshindi alilazimika kupatikana kwa penalti baada ya timu hizo kushindwa kufungana ndani ya dakika 90.
Mpaka kufikia dakika ya 9 kipindi
cha kwanza, Mtibwa Sugar walifanikiwa kupiga shuti moja lililolenga
lango, wakati JKU wao hawakuweza kupiga shuti lolote.
Dakika ya 28, Ally Shomari
iliinyima Mtibwa bao la kuongoza akipiga nje mpira wa krosi uliochongwa
kutoka winga ya kushoto na David Charles Luhende.
Dakika moja baadaye, JKU
walifanya shambulizi zuri, lakini shuti la mshambuliaji hatari Amour
Omary ‘Janja’ lilipaa nje ya lango.
JKU waliendelea kufanya
mashambulizi na katika dakika ya 32 Mohammed Abdallah kutoka winga ya
kushoto alipiga shuti kali lililotemwa na kipa Said Mohamed wa Mtibwa na
mpira kumkuta Mohammed Faki aliyeshindwa kufunga akiwa yeye na goli,
hatimaye Salim Hassan Mbonde akaosha mpira.
Mtibwa waliendelea kuwa katika
wakati mgumu kwani dakika ya 40, Andrew Vicent alishindwa kucheza mpira
mrefu uliopigwa kutoka katikati na ‘Janja’ akaunasa, lakini shuti lake
la mguu wa kushoto lilipanguliwa na Kipa Said Mohammed.
Dakika ya 45, Ally Shomari
alipenyeza pasi nzuri iliyomkuta Ame Ally aliyeachia shuti
lililowababatiza mabeki wa JKU na kuwa kona.
Hata hivyo kona hiyo iliyochongwa na Luhende haikuweza kuzaa matunda.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika hakuna timu iliyoweza kuona lango la mwenzake.
Kwa ujumla katika kipindi cha
kwanza hususani dakika 20 za mwisho, JKU walicheza vizuri kuanzia eneo
la katikati na kutengeneza nafasi nyingi, lakini washambuliaji wake
wakiongozwa na ‘Janja’ hawakuwa na macho ya kuliona lango la Mtibwa.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, lakini washambulizi wa timu zote hawakuwa na mipango sahihi.
Katika dakika ya 82 Ramadhan
Kichuya alikosa goli la wazi akipaisha mpira wa krosi uliochongwa na
Vicent Barnabas aliyeambaa winga ya kushoto akipokea mpira mrefu wa
Salim Mbonde.
Katika dakika za mwisho, Mtibwa
Sugar walipata kona tatu mfululizo, lakini hazikuzaa matunda kutokana na
umakini wa kukaba wa mabeki wa JKU.
Mpaka dakika 90 zinamalizika timu hizo zilitoka suluhu pacha ya bila kufungana na kulazimika kupigwa mikwaju ya penalti.
Wakati huo huo kamati ya
mashindano ya kombe la Mapinduzi 2015 imemtangaza mlinda
mlango wa JKU,
Mohammed Abdulrahman kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo ya kwanza ya nusu
fainali.
Waliopata penalti kwa upande wa
Mtibwa Sugar ni Ally Lundenga, Henry Joseph, Ramadhani Kichuya na Vicent
Barnabas, wakati Luhende alikosa mkwaju wake.
Waliofunga kwa upande wa JKU ni Isihaka Othman, Issa Khaidari, na Khamis Abdallah, wakati Ismail Khamis alikosa tuta lake.
Mtibwa Sugar wanamsubiri mshindi atakayepatikana katika mechi inayotarajia kupigwa usiku huu baina ya Simba na Polisi.
COMMENTS