Kindumbwendumbwe cha michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kinaendelea nchini Equatorial Guinea ambapo mzunguko wa pili ...
Kindumbwendumbwe
cha michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kinaendelea
nchini Equatorial Guinea ambapo mzunguko wa pili uliendelea jana kwa
timu za kundi B kumenyana. Katika mchezo wa awali wa kundi hilo Tunisia
iliinyuka Zambia mabao 2-1. Katika mchezo huo Zambia ndio waliokuwa wa
kwanza kuziona nyavu za Tunisia katika dakika ya 59 likifungwa na
Mayuka. Tunisia iliamka na kusawazisha katika dakika ya 70 kupitia kwa
Akaichi na Chikhaoui akamaliza kazi katika dakika ya 88 kwa kukwamisha
mpira langoni mwa Zambia. Kukosa umakini katika safu ya ushambuliaji na
ulinzi kuliikosesha Zambia ushindi katika mchezo huo.
Katika
mchezo wa pili wa kundi B, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Cape Verde
zilitoka sare ya kutofungana huku kila timu ikishindwa kutumia nafasi
ilizotengeneza kupata magoli. Kwa matokeo hayo Tunisia sasa inaongoza
ikiwa na pointi nne, ikifuatiwa na timu za Cape Verde na DR Congo zenye
pointi mbili kila moja na mkiani ni Zambia yenye pointi moja. Kabla ya
michezo yao ya jana timu hizo zilikuwa na pointi moja kila moja.
Mzunguko
wa pili utaendelea kwa timu za kundi C kupambana. Ghana itaumana na
Algeria, ambapo Afrika Kusini itahenyeshana na Senegal katika mchezo wa
pili wa kundi hilo. Katika mechi za kwanza kwa timu hizo, Algeria
iliizamisha Afrika Kusini kwa mabao 3-1, huku Senegal ikiinyamazisha
Ghana kwa kuichapa 2-1.
Nazo timu za kundi D za Ivory Coast, Mali,
Cameroon na Guinea zitaonyeshana kazi kazi kesho, Jumamosi. Ivory Coast
itaumana na Mali, huku Cameroon ikipambana vikali na Guinea. Timu za
kundi hili zina pointi moja moja kabla ya mpambano wao wa mzunguko wa
pili
COMMENTS