Migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu iliyoanza juzi kuishinikiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwalipa fedha z...
Migomo
ya wanafunzi wa vyuo vikuu iliyoanza juzi kuishinikiza Bodi ya Mikopo
ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwalipa fedha za kujikimu, sasa
imesambaa nchi nzima.
Jeshi
la Polisi Wilaya ya Temeke jana lilitumia mabomu ya machozi kuwatawanya
wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Duce) cha Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam waliokuwa wamekusanyika katika eneo la chuo hicho kwa nia
ya kufanya mgomo na maandamano.
Tukio
hilo lilitokea jana saa 2.00 asubuhi, baada ya polisi kufika katika
eneo hilo wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Bugemwe Melkizedeki, alithibitisha wanafunzi hao kutaka kufanya mgomo.
Hata hivyo, alisema yeye pamoja na viongozi wengine wa serikali ya wanafunzi wakati mgomo huo ukiandaliwa kufanyika.
Alisema wakati huo yeye na viongozi wenzake walikuwa benki wakifuatilia malipo hayo.
Melkizedeki
alisema hadi kufikia saa 4.00 asubuhi jana, wanafunzi wote 3,500
walikuwa wameingiziwa fedha hizo, ambazo ni Sh. bilioni 1.3.
Alisema
katika tukio hilo, wanafunzi nane walikamatwa na polisi, ambao
walipelekwa katika kituo cha polisi Chang’ombe kabla ya kuachiwa kwa
dhamana.
Miongoni
mwa wanafunzi waliokamatwa, ni pamoja na Esau Meshack, anayesoma Kitivo
cha Ualimu, ambaye alisema mgomo huo umeathiri ratiba nzima ya mtihani.
Alisema wakati mgomo huo unafanyika, alikuwa anaingia kwenye mtihani ndipo yeye na wenzake walipokamatwa na polisi.
Meshack
alisema walifikishwa katika kituo hicho cha polisi, ambako
walipekuliwa, huku wakipigwa virungu, makofi kwenye masikio na
kudhalilishwa kwa kuvuliwa nguo.
Wakati
hayo yakijiri, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha
Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam, Kitivo cha Ualimu wa mwaka wa
kwanza wa masomo, wamepanga kufanya maandamano leo. Tofauti na wenzao
wa Duce, maandamano hayo yanalenga kushinikiza kufunguliwa kitivo hicho
chenye wanafunzi zaidi ya 400 baada ya kufungwa kutokana na kudai fedha
za kujikimu.
Mwanafunzi
wa Sayansi ya Ualimu wa Hesabu katika chuo hicho, Mayagi Mustaph,
alisema zaidi ya wanafunzi 400 wanashindwa kuingia darasani kutokana na
chuo kufungwa.
Waziri
wa Fedha wa Serikali ya Wanafunzi hao, Joseph Jingu, alipoulizwa
kuhusiana na hilo, alisema wao kama serikali ya wanafunzi waliuomba
uongozi wa chuo kukifungua kitivo ili kuruhusu wanafunzi kuendelea na
masomo ifikapo Jumatatu ijayo.
Wanafunzi
wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) jana waliandamana kuishinikiza HESLB
kuwapa fedha hizo, ambazo wanadai zimecheleweshwa muda mrefu na hivyo
kuwafanya waishi katika mazingira magumu.
Mtandao
huu ulishuhudia wanafunzi hao wakitaka kuandamana chuoni hapo, huku
wakitamka kuwa kama wasingeingiziwa fedha jana, lazima waandamane
kuelekea kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa.
Askari
wa Jeshi la Polisi walionekana wakirandaranda maeneo ya chuo, kuanzia
saa 2.00 asubuhi hadi saa 6.30 mchana wakiwa na silaha mbalimbali,
yakiwamo maji ya kuwasha, mabomu ya machozi na risasi za moto.
Mkuu
wa Wilaya ya Iringa, Anjelina Mabula, aliwataka wanafunzi hao
kutoandamana, kwani suala lao linafuatiliwa kwa karibu na HESLB.
Kuhusu
wanafunzi 89 wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) waliokamatwa na polisi juzi
na kushikiliwa katika kituo cha polisi cha wilaya mkoani humo, Kamanda
Mungi alisema wameachiwa kwa dhamana.
Wanafunzi
wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wamegoma kushinikiza serikali kupatiwa
fedha hizo pamoja na kulalamika kukatwa fedha nyingi kwa ajili ya Bima
ya Afya.
Mgomo
huo ulianza juzi usiku na kuendelea hadi jana kwa wanafunzi wa Kitivo
cha Elimu, Kozi Maalumu kwa ajili ya walimu wa masomo ya sayansi na
hisabati pamoja na Kitivo cha Sanaa ya Lugha na Sayansi ya Jamii.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti mbele ya viongozi waliotumwa na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, kusikiliza madai yao, wanafunzi hao walisema wanashindwa
kuingia madarasani kutokana na hali ngumu waliyo nayo.
Waziri
wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi katika Kitivo cha Elimu, Mpandalume
Simon, alitaja sababu za mgomo huo kuwa ni kuishinikiza serikali
kusikiliza kilio chao cha kucheleweshewa fedha hizo.
Alitaja
madai mengine kuwa ni kukatwa Sh. 100,000, lakini vyuo vikuu vingine
wanalipa Sh. 50,400 kwa ajili ya huduma ya bima ya afya.
Akizungumza
na wanafunzi hao, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa, alisema
serikali imesikia kilio chao na ndio maana waziri mkuu aliwatuma
kuwasikiliza kutokana na yeye kubanwa na majukumu ya kiserikali
bungeni.
“Kabla
ya kuonana na nyie tumepita utawala wa chuo na wamethibitisha juu ya
malalamiko yenu na wanasubiri fedha zikishafika, watahakikisha ifikapo
Jumatatu zitakuwa tayari chuo,” alisema Galawa.
Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Stephen Kebwe, alisema amefika na
viongozi wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na Mganga Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma ili kusikiliza malalamiko hayo.
Hata
hivyo, baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao walijikuta katika wakati
mgumu baada ya kuzomewa na wanafunzi na kulazimika kukatisha mazungumzo
bila kufikia mwafaka wakidai hawawataki, wanamtaka waziri mkuu mwenyewe.
COMMENTS