Zacharia Hanspoppe MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya timu ya Simba Zacharia Hansp...
Hanspoppe alisema jana hawajutii makosa yao ya kuamua kubadilisha mkuu wa benchi la ufundi kwa kumuondoa kocha Patrick Phiri wa Zambia na kumleta Goran Kopunovic raia wa Serbia ambaye ndiye aliyeiongoza timu hiyo kuipa ubingwa wa kombe la Mapunduzi Jumanne iliyopita na kuongeza kuwa wanaimani atawapa mafanikio zaidi.
“Kamwe hatuwezi kujutia maamuzi yetu kwa kumtoa Phiri na kumleta Kopunovic kwa sababu kila mtu ameona mabadiliko yaliyoonyeshwa na timu yetu kwa muda mfupi ambayo Mserbia huyo amekaa nayo kwenye michuano ya Mapinduzi,”alisema.
Alisema kutokana na mabadiliko yaliyo oneshwa na timu yao wanauhakika wa kupata ushindi katika mechi za Ligi Kuu ambapo mpaka sasa wako katika nafasi ya 12 kwenye msimao wa ligi hiyo wakiwa na pointi 12.
“Hatuna hofu baada ya kuona uwezo wa kocha Kopunovic kupitia michuano ya Kombe la Mapinduzi ninaimani kila mwanachama na shabiki wa Simba atakuwa amevutiwa na uwezo wake cha msingi tumpe sapoti ili azidi kuijenga timu yetu ili ifanya vizuri msimu huu,” alisema Hans Poppe.
Kiongozi huyo alisema baada ya kuridhishwa na mwenendo wa timu yao watahakikisha wanampatia kila anachokihitaji kocha huyo ilimradi kikosi chao kirudi katika hali yao ya zamani na kupigania ubingwa wa Tanzania bara msimu huu.
“Mwenyewe Kopunovic ametuambia kuwa Simba bado inayo nafasi ya kuwania ubingwa wa Tanzania bara msimu huu na baada ya kutuambia hivyo tumejiandaa kuhakikisha kumpatia kila kinachowezekana ili kumpa urahisi wa kufikia kile anachokihitaji msimu huu,”alisema Poppe.
Aidha, aliwataka wachezaji wa timu hiyo kutobweteka na ubingwa wa kombe la Mapinduzi na kuendelea kujituma na kusikiliza kwa makini maelekezo wanayopewa na makocha wao ili Simba ibadili mwenendo wake wa kusuasua kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania bara.
Poppe alisema ili kuhakikisha wachezaji wao wanakuwa na ari zaidi wamewapatia wachezaji wao milioni 10, iliyokuwa zawadi ya ubingwa wa kombe la Mapinduzi ili wagawane pamoja na viongozi wao wa benchi la ufundi.
COMMENTS