TIMU ya Soka ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars imefuzu kucheza fainali za michezo ya Afrika, baada ya kuifunga Zambia wana Shipolopolo bao...
TIMU ya Soka ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars imefuzu kucheza fainali za michezo ya Afrika, baada ya kuifunga Zambia wana Shipolopolo bao 4-2.
Katika mchezo huo uliochezwa Lusaka, Zambia na kuhudhuriwa na maelfu ya Watanzania wa nchini humo, Twiga kipindi cha pili ilicheza kwa kujiamini na kuutawala mchezo.
Shipolopolo ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata goli katika kipindi cha kwanza na hadi timu zinaenda mapumziko Zambia ilikuwa ikiongoza 1-0.
Baada ya kurejea kutoka mapumziko, Twiga ilionekana ikicheza kwa ari mpya ambapo dakika moja tu baada ya kuanza kwa kipindi hicho, ilisawazisha bao hilo la Zambia kupitia mchezaji wake Asha Rashid.
Twiga iliendelea na jitihada za kusaka mabao ambapo dakika ya 51 mchezaji Sherida Boniface alitumbukiza kimiani bao la pili na hivyo kuongeza hamasa ya mchezo miongoni mwa wachezaji wa Twiga.
Wachezaji wa Twiga waliendelea kulisakama goli la Shipolopolo na kupata bao jingine la tatu kupitia mchezaji wake Ilo Mulezi, dakika ya 70.
Huku washangiliwa na mashabiki waliokuwapo uwanjani hapo, Twiga zikiwa zimebakia dakika tano mchezo kumalizika iliongeza bao la nne kupitia mchezaji wake, Sophia Mwasikili.
Akizungumzia ushindi huo wa jana, Mkuu wa msafara huo ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) na Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Soka ya Wanawake, Blassy Kiondo alisema jitihada za wachezaji na viongozi kwa ujumla zimewezesha ushindi huo.
“Huu ni ushindi kwa Watanzania wote kwa ujumla kwa kuwa timu hii imejitahidi kucheza kwa hali na mali na kuonesha ni kwa kiasi gani inaweza kumudu mikikimikiki iliyokutana nayo huku,” alisema Kiondo.
Aliongeza kuwa licha ya kukutana na vikwazo kadhaa, lakini wachezaji hao hawakukata tamaa na badala yake walijituma kwa hali na mali na hatimae kuiletea Tanzania sifa.
COMMENTS