Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi akiwania mpira na kipa wa Ruvu Shooting, Abdallah Rashid na beki wa timu hiyo, Hamisi Kasanga waka...
Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi akiwania mpira na kipa wa Ruvu Shooting, Abdallah Rashid na beki wa timu hiyo, Hamisi Kasanga wakati wa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana. Simba ilishinda 3-0. (Picha na Fadhili Akida).
BAADA ya timu za Azam na Simba kupata ushindi katika mechi zao walizocheza jana, kiti cha Yanga kinaanza kuonekana kuwa cha moto kutokana na timu hizo mbili kuifukuzia kwa karibu.
Simba jana ilijipatia ushindi wa 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting huku Azam ikijipatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union. Yanga ambayo kwa sasa inaongoza ligi kwa kuwa na pointi 37, imeiacha Azam kwa pointi moja na Simba kwa pointi 5.
Azam inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 36 na Simba ina pointi 32. Katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilipata magoli yake yote matatu kipindi cha pili baada ya kushindwa kutumia vema nafasi ilizopata kwenye kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili kilipoanza Simba iliingia kwa kishindo na dakika ya 58 walipata bao la kwanza kwa njia ya penalti iliyopigwa kiufundi na mchezaji wake Ibrahim Ajibu. Katika mkwaju huo, kipa alienda kushoto wakati mpira ukimiminika kulia.
Penalti hiyo ilisababishwa na beki wa Ruvu Shooting aliyemchezea madhambi kiungo mshambuliaji wa Simba, Awadh Juma ndani ya eneo la penalti ambaye aliingia kipindi cha pili. Dakika tatu baadae, Simba ilijipatia goli lake jingine kupitia Awadh Juma baada ya kuwapiga chenga mabeki wa Ruvu Shooting na kupiga shuti la mbali.
Simba yenye pointi 32 kwa sasa ikiwa inashika nafasi ya tatu iliendelea na harakati za kusaka magoli na dakika ya 75 iliongeza bao jingine kupitia mchezaji wake Elias Maguli.
Mchezaji huyo alifunga bao hilo kutokana na pasi safi aliyopewa na Said Ndemla. Mchezaji Emmanuel Okwi katika mchezo huo wa jana alishindwa kutamba hasa baada ya kukosa mabao ya wazi katika kipindi cha kwanza.
Iwapo mchezaji wa Ruvu Shooting, Yahya Tumbo angetumia vema nafasi aliyoipata dakika 55 ya kufunga goli, angekuwa ameisaidia timu yake hiyo kujipatia goli la kufuta machozi.
Katika mchezo huo wa jana katika kipindi cha kwanza Simba ilionekana kutotulia mkazo mchezo huo na hasa pale wachezaji wake walipokuwa wakishindwa kutumia vema nafasi walizozipata.
Azam kwa upande wake, ilijipatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Azam ilijipatia bao lake la kwanza kupitia mchezaji wake John Bocco dakika ya 31, kutokana na pasi nzuri kutoka kwa mchezaji Mudathir Yahaya. Coastal Union ilicheza bila ya wachezaji wake, Godfrey Wambura, Fikirini Bakari na kipa wake, Shaban Kado.
COMMENTS