Lowassa Akiongea na wananchi Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akiwasalimia wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya mjini Do...
Mbunge
wa Monduli, Edward Lowassa akiwasalimia wanafunzi kutoka vyuo
mbalimbali vya mjini Dodoma na waendesha bodaboda walioandamana kwenda
nyumbani kwake mjini humo jana kwa ajili ya kumshawishi achukue fomu ya
kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kadri uchaguzi mkuu unavyokaribia ndivyo makundi mbalimbali ya jamii yanavyoibuka kwa staili tofauti za kuwashawishi baadhi ya makada ili watangaze nia ya kuwania urais ndani ya CCM.
Makundi
hayo yalianza kwa kumshawishi Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na sasa
yameibuka mengine katika mikoa ya Mbeya na Arusha yakiwashawishi Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Hata
hivyo makundi hayo yameelezwa na mmoja wa watu waliotangaza kuwania
nafasi hiyo kuwa ni mbinu ya kimaigizo ya baadhi ya wagombea kujitangaza
kwa kuyaandaa na kuyalipa posho.
Wanafunzi watinga kwa Lowassa
Siku
moja baada ya kuwapokea masheikh 50 kutoka Bagamoyo, jana mbunge huyo
alipokea makundi ya wanafunzi wa vyuo vikuu, madereva wa pikipiki
(bodaboda) na wamachinga wa Dodoma wakimtaka achukue fomu kuwania nafasi
hiyo.
Tayari
mbunge hiyo alishampokea Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Dk
Rapahel Chegeni na baadaye kundi marafiki wa Lowassa kutoka mikoa ya
Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Wanafunzi
hao ambao waliongozana na baadhi ya wahadhiri walitoka Chuo Kikuu cha
Dodoma (Udom), St John, Mipango na Chuo cha Biashara (CBE), Tawi la
Dodoma.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti nyumbani kwake mjini hapa jana, wanafunzi hao
walimtaka Lowassa kuchukua fomu ya kuwania urais wakati utakapofika.
“Sisi
hatutafuni maneno, ni watu wawazi na tuna tamaa kwa mtu ambaye tuna
matumaini naye na mtu ambaye tuna matumaini naye ni wewe Lowassa,”
alisema Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wazazi la CCM Kusini Unguja, Haji
Amiri na kuongeza:
“Watanzania wana matumaini na wewe. Sasa yeyote anayetaka kuyafunika matumaini yale ni sawa na kukiuka matumaini yetu.”
Kiongozi
wa madereva Bodaboda, Bakari Ndalama alisema yeye na wenzake walifika
kumuomba kugombea nafasi hiyo kwa sababu akichukua, hali ya ajira
itakuwa nzuri.
“Wewe umekuwa ukilisemea jambo hili mara kwa mara. Ukipata urais ajira zitakuwa nzuri kwa vijana,” alisema Ndalama.
COMMENTS