Rais Mahmoud Abbas wa Palestina (kulia) akisaini Mkataba wa Rome unaounda Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Palestina ku...
Rais Mahmoud Abbas wa Palestina (kulia) akisaini Mkataba wa Rome unaounda Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Palestina kuwasilisha ombi la kujiunga ICC
Palestina inatazamiwa kuwasilisha rasmi maombi ya kujiunga na Mahakama
ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kufuatia hatua ya Rais Mahmoud Abbas
kusaini mkataba wa mahakama hiyo mjini The Hague.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliitolea wito ICC kulikataa ombi la Palestina kujiunga na mahakama hiyo, aliloliita la kinafiki. Kwa mujibu wa Netanyahu, serikali ya Mamlaka ya Palestina si dola, bali kundi lililounda ushirikiano na kundi jengine la kigaidi, Hamas, ambalo linafanya uhalifu wa kivita.
"Israel ni dola linalofuata sheria na lenye jeshi lenye maadili linaloheshimu sheria zote za kimataifa. Tutawalinda wanajeshi wetu kama wao wanavyotulinda sisi." Ilisema taarifa iliyotolewa na ofisi ya Netanyahu, baada ya kikao cha dharura kwenye makao makuu ya wizara ya ulinzi hapo Alhamisi.
Siku ya umatano, Rais Abbas alisaini mkataba wa ICC na makubaliano mengine 19 ya kimataifa, kufuatia hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku moja nyuma, kulikataa pendekezo la Palestina kuitaka Israel ikomeshe ukaliaji wake kufikia mwaka 2017.
.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
Marekani, Israel zakasirika
Marekani na Israel zilichukizwa sana na hatua ya Abbas kusaini mkataba huo, ambapo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Jeffrey Rathke, alisema ni hatua isiyo na manufaa kabisa, na ambayo haipiganii matakwa ya Wapalestina ya kuwa na dola huru yenye mamlaka kamili.
Kwa mujibu wa kanuni za ICC, uwanachama wa Palestina utairuhusu mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi, kuchunguza tuhuma za uhalifu wa kivita uliotendwa ndani ya ardhi ya Palestina, bila ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambako Israel inakingiwa kifua na Marekani.
Ingawa Israel si mwanachama wa mahakama hiyo, raia wake wanaweza kushitakiwa kwa matendo yao katika ardhi ya Wapalestina.
Chanzo DW
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/dpa/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba
COMMENTS