Raisi Jakaya Kikwete RAIS Jakaya Kikwete amesema uhusiano wa Tanzania na Msumbiji ni wa kipekee na kindugu hivyo utaendelea kudumishwa...
Kikwete alisema hayo juzi muda mfupi baada ya kuwasili mjini Maputo kwa ajili ya kuhudhuria kuapishwa kwa Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi na kupokea taarifa ya Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Shamsa Nyanduga.
Alisema Tanzania na Msumbiji ni washirika na zina ushirikiano, hivyo hauwezi kupotea hasa wakati huu ambapo kuna ugunduzi wa mambo mazuri pande zote, ikiwa pamoja na suala la gesi.
“Tuna ushirikiano wa muda mrefu na Msumbiji, hawa ni ndugu na rafiki zetu tumetoka nao mbali na hata chama cha Frelimo kimeundiwa Dar es Salaam, ni rahisi kuendeleza ushirikiano nao katika masuala mbalimbali ya maendeleo na kudumisha uhusiano wetu mzuri,”’ alisema Balozi Nyanduga akitoa taarifa ya ubalozi kwa Rais Kikwete, alisema uhusiano kati ya Tanzania na Msumbiji ni imara na wa kindugu.
Aidha, Balozi Nyanduga alisema uhusiano kati ya vyama tawala vya CCM na Frelimo ni mzuri na kuongeza kuwa katika kuimarisha uhusiano zaidi, Rais Nyusi alipoteuliwa na Frelimo kuwa mgombea urais, alifanya ziara ya kujitambulisha nchi za nje, kwa kuanzia na Tanzania kuonesha mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Msumbiji.
Alisema viongozi wa ngazi mbalimbali wa serikali na CCM na Frelimo, wamekuwa wakitembeleana na kuna mafanikio makubwa ya uhusiano huo wa kisiasa. Lakini alisema uhusiano wa kiuchumi na kibiashara, bado ni mdogo, licha ya ujirani na muingiliano mkubwa wa wananchi pande zote.
Balozi Nyanduga alimweleza Rais kuwa licha ya sherehe hizo za kuapishwa Rais Nyusi, bendera za nchi hiyo zinapepea nusu mlingoti baada ya watu 79 kufa na 154 kulazwa hospitalini baada ya kunywa pombe ya kienyeji, iliyosadikiwa kutiwa sumu ya mamba katika mkoa wa Tete.
COMMENTS