YANGA leo itakuwa mwenyeji wa Azam FC katika mechi ya raundi ya nane ya Ligi Kuu bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Sa...
YANGA leo itakuwa mwenyeji wa Azam FC katika mechi ya raundi ya nane ya Ligi Kuu bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Timu zote zinashuka dimbani zikiwa na pointi 13 kila moja zikitofautiana kwa uwiano wa mabao.
Mechi ya leo ni ya pili kukutana kwa timu hizo msimu huu, baada ya ile ya Ngao ya Jamii iliyofanyika mapema Septemba na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 yaliyofungwa na aliyekuwa mchezaji wao Geilson Santos ‘Jaja’ na Simon Msuva.
Katika historia ya kukutana kwao kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, Yanga wanaonekana kuwazidi Azam baada ya msimu wa mwaka 2012/2013 kuwafunga bao 1-0.
Aidha, katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi msimu uliopita Azam iliifunga Yanga mabao 3-2 wakati kwenye mchezo wa pili walitoka sare ya mabao 2-2.
Hivyo mechi ya leo inatarajiwa kuwa ya vuta nikuvute kwani ni wazi kuwa mabingwa watetezi Azam watataka kulipiza kisasi huku Yanga wakitaka kuendeleza ubabe.
Yanga inaingia uwanjani ikiwa imefanya mabadiliko kwenye benchi lake la ufundi kwa kumtimua kocha Marcio Maximo aliyeanza kuifundisha timu hiyo tangu mwanzoni mwa msimu na kuwarejesha Hans van der Pluijm na Charles Mkwasa.
Kwa upande wa Azam Fc Joseph Omog bado anaendelea kushika usukani huku kocha msaidizi wake akiwa ni George ‘Best’ Nsimbe raia wa Uganda aliyechukua mikoba ya Kally Ongala.
Kila timu ilifanya usajili katika dirisha dogo ambapo Azam iliwasajili beki wa Ivory Coast, Paschal Wawa lakini pia winga wa kimataifa wa Uganda Brian Majwega wakati Yanga ikiwaongeza Amis Tambwe, Mliberia Kpah Sherman, na Danny Mrwanda.
Timu zote zilikuwa katika maandalizi ambapo Azam ilikuwa Uganda na Yanga ilienda Bagamoyo.
Makocha wote wametamba kuibuka na ushindi leo, kocha Omog akisema hakuna cha kuizuia kuifunga Yanga huku kocha Pluijm akitamba kutumia mfumo wa ushambuliaji na kuhimiza wachezaji wake kujiamini ili kuibuka na ushindi.
COMMENTS