WAZIRI wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa, ameagiza wataalamu kutayarisha mwongozo kwa ajili ya kampuni za simu,...
WAZIRI wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa, ameagiza wataalamu kutayarisha mwongozo kwa ajili ya kampuni za simu, utakaoelekeza jinsi ya kutuma meseji katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.
Prof. Mbarawa, alisema hayo jana alipokuwa akifungua mkutano wa kuadhimisha siku ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Jumuiya ya Mawasiliano Afrika, jijini Dar es Salaam, ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Waziri Mbarawa, alisema mwakani ni kipindi cha uchaguzi mkuu, hivyo kuna baadhi ya watu wamekuwa wakitumia simu kutuma meseji ambazo zinaweza kuhatarisha usalama wa raia.
“Watu wanaotuma meseji hizo, nimeshawaagiza wataalamu kutoka wizarani na TCRA kwa ajili ya kuandaa mwongozo huo kwa ajili ya kutuma meseji, kwa sababu teknolojia imekua, watu wanaweza kuitumia vibaya,” alisema.
Vilevile, alivitaka vyombo vya habari vitumike kuwaelimisha wananchi vizuri kuhusu masuala ya uchaguzi, kwa kutahadharisha kuwa mwongozo walioupata usiwe kwenye makaratasi tu bali wautekeleze.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Prof. John Nkoma, alisema kuwa, hivi sasa Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kuwa wanaotumia kadi za simu ni milioni 28, mtandao wa mawasiliano ni milioni tisa ikiwa ni pamoja na ukuaji wa huduma za simu ambazo zimewezesha watu kutuma na kupokea fedha.
Pia, alisema serikali imewekeza dola milioni 200 katika mkongo wa taifa kwa ajili ya maboresho kwenye upande wa utangazaji.
COMMENTS