TAFSIRI NA UKALIMANI

Tafsiri na ukalimani

  DHANA YA TAFSIRI.

Tafsiri imefasiliwa kuwa, ni kutoa mawazo kutoka katika lugha moja kwenda lugha nyingine bila ya kubadilisha maana. [TUKI 2002]

Mwansoko na wenzake (2006), wanafasili tafsiri kuwa ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja kwenda lugha  nyingine.

Catford [1965:20] anasema tafsiri ni, “Kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja {lugha chanzi/ LC} na kuweka badala yake mawazo yanayolingana na hayo kutoka lugha nyingine {lugha lengwa/ LL}.

Mshindo (2010:2) ansema kufasiri ni kufafanua maana ya matini moja na kutayarisha baadae matini nyingine inayowiana nayo ambayo huitwa tafsiri na ambayo inawakilisha ujumbe uleule uliomo katika matini ya awali kwa kutumia lugha nyingine.

Newmark (1982) Tafsiri ni jaribio la kuwasilisha ujumbe uleule ulio andikwa katika lugha moja kwa lugha nyingine.

AS-Safi akimnukuu Dubois (1974), anaeleza kuwa tafsiri ni uelezaji katika lugha nyingine au lugha lengwa wa kile kilichoelezwa katika lugha nyingine (lugha chanzi) ikihifadhi maana na mtindo wa matini chanzi.

Nida na Taber (1969), tafsiri ni uzalisha upya ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe asili vya lugha lengwa (LL) vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi, kwanza kimaana na pili kimtindo.

Larson (1984), tafsiri inahusisha uhawilishaji wa maana iliyoko katika maandishi katika lugha chanzi kwenda katika lugha lengwa.
            Maana zote hizo tulizoziangalia, utaona kuwa, kuna mambo matatu muhimu yanayojitokeza, mambo hayo ni:
(i) Ujumbe/Mawazo u/yanayotakiwa kutafsiriwa sharti yawe katika maandishi.
(ii) Mawazo au ujumbe kati ya lugha chanzi na lugha lengwa sharti yalingane.
(iii) Tafsiri inaweza kuwa kutoa maana ya maneno au mawazo.

Kutokana na fasili hizo tunaweza kusema kuwa;
Tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo, ujumbe, au taarifa iliyopo katika maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa bila kupoteza maana ya msingi na mtindo uliotumika katika matini chanzi.


HISTORIA NA MAENDELEO YA TAFSIRI

Wanjala (2011), anaeleza kuwa historia ni taarifa, maelezo na uchambuzi wa matukio, watu na nyakati teule zinazoathiri maisha ya wanajamii husika, sasa na hata siku za usoni. Matukio hayo huteuliwa sawia waasisi au mashujaa wa asasi hizo. Ujuzi wa historia hutuwezesha kudhibiti, na kuthamini, misingi na maendeleo ya taaaluma zetu. Kwa kurejelea ujuzi huo, pia tunaweza kubashiri mwenendo wa siku za usoni.



Ufafanuzi wa kihistoria huendelezwa kupitia vipindi bainifu vya tajiriba ya binadamu. Historia ya tafsiri imeangaliwa kwa kuegemea vipindi muhimu vya maendeleo na mabadiliko ya elimu na utamaduni. Vipindi vilivyojitenga wazi ni vitano:



                                              👉 Enzi za kale (Old Ages)
                                             👉 Enzi za giza (The dark Ages)
                                              👉Enzi za ufufuko (Renaissance period)
                                             👉  Enzi za kati (Middle Ages)
                                              👉Enzi za sasa (Late Ages)
p    Soma historia na maendeleo ya tafsiri kwa undani zaidi hapa
                                 
                        
TAFSIRI NA UKALIMANI.Pdf

                                         

                                             NADHARIA YA TAFSIRI

Katika mada hii tutajikita kwa kuangalia kwa ufupi maana ya nadharia ya tafsiri, dhima, aina na sababu za kuanzishwa kwa nadharia ya tafsiri.


     Nadharia ni nini?

Kwa mujibu wa Mdee na wenzake (2011) wanafasili nadharia ya tafsiri kuwa ni mpango wa mawazo uliotungwa ili kueleza jinsi ya kufanya au kutekeleza jambo Fulani.

Vilevile Sengo (2009:1) anafasili nadharia kuwa ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu ,watu au jamiii ya pahala Fulani kwa sababu fulani.



Nadharia ya tafsiri


Kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2013:7) nadharia ya tafsiri ni nguzo au muhimili wa nguzo ya tafsiri. Ni msingi wa kazi zote za tasiri. Nadharia ya tafsiri ni maeleo kuntu juu ya vipengele vinavopaswa kuzingatiwa na kila mfasiri kila akabiiwapao na kazi ya kutafsiri.
Naye Wanjala (2011:167)., anasema kuwa nadharia ya tafsiri huchunguza mbinu muafaka za kutumika katika mchakato wa kutafsiri kwa ufanisi matini ya aina Fulani mahsusi. Ni jumla ya mawazo au maarifa katika mchakato wa kufasiri; misingi na kanuni za jumla pamoja na miongozo, mapendekezo na vidokezo muhimu.
Kwa kuhitimisha juu ya dhana ya nadharia ya tafsiri tunaweza sema kuwa ni mawazo au muhimili unaomuongoza mfasiri juu ya vipengele muhimu anavyopaswa kuvishughulikia katika mchakato wa kufasiri kutoka matini chanzi kwenda matini lengwa.

Sababu za kuanzishwa kwa nadharia za tafsiri.

Newmark (1982), Mwansoko na wenzake (2006) wanasema kuna mambo matatu yaliyosababisha kuanzishwa kwa nadharia ya tafsiri ambayo ni: -
Kwanza, wingi wa makosa katika tafsiri zilizochapishwa awali. Ilionekana kwamba kulikuwa na makosa mbalimbali kama vile makosa ya kimuundo, kimaumbo, kimsamiati pia ilikuwa ni nadra kupata tafsiri zisizokuwa na makosa.
Mfano: When did the rain start beating us?
Tafsiri: Ni lini mvua ilianza kutupiga?
                        Terms and condition to apply
Tafsiri: Vigezo na masharti kutumika
Kulingana na mifano hiyo ambayoinaonekana kuwa na  makosa ya kimuundo, kimsamiati na kimaana kwa lugha zote mbili yaani lugha chanzi na lugha lengwa. Hivyo mifano hiyo ilitakiwa ionekane katika muundo ufuatao;
             Mfano: When did the rain start rained us?
                          Ni lini mvua ilianza kutunyeshea?
                          Terms and condition to be applied
                          Vigezo na masharti kuzingatiwa         
Pili, kuwepo kwa idadi kubwa (na inayoongezeka) ya mashirika na asasi zinazojishughulisha na kutafsiri matini mbalimbali. Mashirika haya pamoja na watu binafsi walizua utata kwani walifasiri kwa namna tofauti matini zinazofanana. Mifano ya mashirika au taasisi hizo ni kama vile Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Tasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), Shirika la habari la Tanzania pamoja na mashirika ya watu binafsi yanayofundisha wageni lugha ya Kiswahili. Kutoana mtafaruku huo ukazua sababu za kuzinduliwa kwa nadharia ya tafsiri ili kuweka kanuni na vigezo vinavyofanana katika kutafsiri dhana mbalimbali.  
      
Tatu, mfumuko wa istilahi katika taaluma mbalimbali hususani sayansi na teknolojia, hivyo basi hali hii ikazua haja ya kusanifisha istilahi hizi katika lugha lengwa  na chasili
            Mfano:    Kiingereza               Kiswahili
                            Computer                Tarakilishi                    
                            Calculator               Kikokotozi                
                            Memory card           Kadi sakima
                            Windows                  Kiweo    
                            Simcard                    Kadiwia/Mkamimo
                             ATM                       Kiotomotela
Hali hii ilihitaji nadharia ili wafasiri waongozwe na kanuni moja wanapofasiri. Hivyo nadharia ya tafsiri ilianzishwa kwa lengo la kuleta ulinganifu wa istilahi hizo kati ya lugha moja na nyingine ili kuwe na ufanisi zaidi.

Dhima za nadharia ya tafsiri

Dhima za nadharia ya tafsiri ni kama zifuatavyo;
Kuonesha mbinu ambazo zinazofaa kutumiwa  kufasiria aina mbalimbali za matini. Nadharia hizi za tafsiri husaidia au humpa muongozo mfasiri kujua mbinu muhimu ambazo hazina budi kufuatwa wakati wa kutafsiri matini yoyote. Mfano wa mbinu hizo ni pamoja na tafsiri ya neno-kwa-neno, tafsiri sisisi, tafsiri ya kisemantiki na tafsiri ya kimawasiliano. Kati ya mbinu hizo mbinu ambazo hutumika zaidi ni tafsiri ya kisemantiki na tafsiri ya kimawasiliano hii ni kwa sababu mbinu hizi ndizo zinakidhi malengo makuu ya tafsiri. Malengo hayo ni kutoa taarifa na iktisadi ya lugha.  
    
Pili, kutoa misingi, kanuni,  sheria na vidokezo vya kufasiri matini na kuhakiki tafsiri, yaani matini zilizokwisha tafsiriwa. Vilevile nadharia za tafsiri humsaidia mfasiri kujua misingi, kanuni, sheria na kuhakiki matini mbalimbali za tafsiri ili kuweza kutupatia tafsiri zilizo bora. Mfano wa mambo muhimu ambayo hayana budi kuzingatiwa wakati wa mchakato wa uchambuzi wa matini ni; kwanza, kusoma matini nzima. Katika usomaji wa matini nzima dhumuni lake ni kubaini lengo la matini, kubaini lengo la mfasiri, kubaini wasomaji lengwa , umbo la matini lengwa na kubaini mtindo wa matini chanzi. Pili, kusoma matini mara ya mwisho. Pia kuna hatua (vidokezo) muhimu vya kufuata kama vile, maandalizi, uchambuzi, uhawilishaji, kusawidi rasimu ya kwanza, kudurusu rasimu ya kwanza ili kupata rasimu ya pili, kusomwa rasimu ya pili na mtu mwingine na kusawidi rasimu ya mwisho.

Tatu, kueleza jinsi ya kuvishughulikia vipengele vidogovidogo katika tafsiri kma vile maana na umuhimu wa vistari, nukta, mkato, italiki, makosa ya uchapaji na mambo mengine kwa ujumla. Kwa mfano maana na nguvu za taarifa zinazobebwa na sitiari, uwasilishaji katika matini wa maudhui na fani yote haya yana uzito sawa na mazingatio mengine ya zoezi  la tafsiri.
                        Mfano Asiyejua utu si mtu.
Katika mfano huo neno utu litatiliwa mkazo katika mchakato wa tafsiri tofauti na maneno mengine yaliyo katika matini hiyo.

Nadharia mahususi za tafsiri/Aina za nadharia ya 
tafsiri

Zifuatazo ni aina za nadharia ya tafsiri, tutaangalia nadharia ya usawe wa kimuundo, nadharia ya usawe wa kidhima, nadharia ya usawe wa aina-matini, na nadharia changamani.
Nadharia ya Usawe wa Kimuundo; Nadharia hii inatetewa na mtaalam Catford (1965) Anasema kwamba, tunapofanya kazi ya kutafsiri ni muhimu kuzingatia ulinganifu wa kimuundo kati ya matini chanzi na matini lengwa hii ina maana kwamba, muundo wa matini chanzi ujitokeze katika matini lengwa. Hivyo katika nadharia hii muundo ni muhimu. Pia nadharia hii hutumika zaidi katika kutafsiri maandiko ya kidini hasa Biblia.
Nadharia ya usawe wa kidhima; waasisi wa nadharia hii ni pamoja na Nida (1964) na Nida na Taber (1969) wanaona kuwa usawe wa kidhima ni muhimu zaidi kuliko usawe wa kimuundo. Wanaendelea kueleza kuwa wafasiri wanapaswa kuhakikisha kwamba dhima ya matini chanzi pamoja na athari zake zinajitokeza katika matini lengwa. Yaani kama matini chanzi inawalenga watoto inapaswa iandikwe kiasi kwamba watoto wataweza kuelewa. Pia kwa kuzingatia nadharia hii unapaswa kutumia lugha rahisi na inayoeleweka na watu wote. Vilevile tafsiri yako iwe nzuri kiasi kwamba mtu atakaposoma asiweze kugundua kwamba hiyo kazi imetafsiriwa.
Nadharia ya usawe wa aina-matini; Watetezi wa nadharia hii ni Reiss (1971), Bülher na Newmark (1982) wanasema kuwa matini yoyote ile inapaswa kufasiriwa kwa kuzingatia aina yake. Hii ina maana kwamba kazi itakayotokea (matini lengwa) ifanane na matini chanzi. Mfano kama matini chanzi ni ya kisheria itakapotafsiriwa matini lengwa nayo ionekane kuwa ya kisheria. Kinachozingatiwa katika nadharia hii ni fani (muundo) na maudhui (dhima/lengo) ya matini yenyewe inayotafsiriwa.
Nadharia Changamani, Nadharia hii iliasisiwa na P.S. Malangwa (2010) nadharia hii inadai kwamba huwezi kufanya tafsiri kwa kutumia nadharia moja tu, kwa sababu hakuna nadharia inayojitosheleza yenyewe. Hivyo basi nadharia hii ni mjumuisho au hujumuisha nadhari nyingine ili kuleta tafsiri inyojitosheleza.
Hivyo nadharia ya tafsiri imechangia kuleta tafsiri bora kwani husaidia katika kuweka wazi misingi na vipengele muhimu vya kuzingatiwa katika mchakato mzima wa kutafsiri, vigezo hivi huwasaidi wafasiri kuwa na mwongozo sawa wa mambo ya kuzingatia ili kuepuka tafsiri zenye makosa.


SIFA ZA MFASIRI BORA
Mfasiri bora anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:
Ø  Awe mahiri wa lugha husika, hii ina maana kuwa awe anajua kwa ufasaha lugha zote mbili, yaani lugha chanzi na lugha lengwa. Hii ni kujua vizuri nyanja mbalimbali za Isimu ya lugha husika kama vile; Fonolojia-{Matamshi}, Mofolojia-{Maumbo}, Sintaksia-{Muundo} na Semantiki-{Maana}
Ø  Awe na ufahamu mkamilifu wa ujumbe au mada iliyoandikwa katika matini chanzi na uwezo au jinsi ya kuelezea ujumbe au mada hiyo kwa ufasaha katika lugha lengwa.
Ø  Awe mjuzi wa TEHAMA.
Ø  Ajue lugha mbili au zaidi.
Ø  Awe na tajiriba kubwa ya usomaji wa aina mbalimbali za tafsiri na kujiendeleza kulingana na mabadiliko ya kijamii.
Ø  Afahamu vizuri watu, jamii na utamaduni wa watumiaji wa lugha chanzi na lugha lengwa.
Ø  Afahamiane na watu wengi, yaani kujichanganya changanya na watu wa fani au sekta mbalimbali.
Ø  Awe na tabia yakushirikiana na watu wengine katika shughuli za kufasiri.

 

MADILI YA MFASIRI BORA

        i.            Uaminifu, mfasiri bora anapaswa kuwa mwaminifu moja kwa moja kwa mteja wake na matini anayoitafsiri.
      ii.            Anayejituma na kufanya kazi kwa bidi
    iii.            Anapaswa kuelewa na kuzingatia tartibu za kazi zake. Mfano makubaliano na mteja yawe kwa mkataba wa maandisi ambao utataja mteja ni nani au taasisi, mfasiri, aina ya kazi, lugha asilia, idadi ya kurasa, taratibu za malipo pamoja na kiwango pia kazi hiyo itakamilika baada ya muda gani.
    iv.            Mfasili bora ni yule ambaye ana ushirikiano na wafasili wenzake na watu wa sekta nyingine.
      v.            Aepuke vishawishi, yaani asiwe na tamaa awe na msimamo. {asijipendekeze wala kujishusha kwa mteja}
    vi.            Awe nadhifu, yaani nadhifu wa moyo na muonekano.


UMUHIMU WA TAFSIRI

Tafsiri ina dhima zifuatazo:
§  Ni njia ya mawasiliano
§  Nyenzo ya kueneza utamaduni kutoka jamii moja hadi nyingine.
§  Mbinu ya kujifunza lugha za kigeni.
§  Mbinu ya kukuza lugha.
§  Ni kiliwazo cha mfasiri.
§  Njia ya kuongeza kipato.{Kiuchumi}

Mawasiliano ni nguzo kuu ya uhai, maelewano na maendeleo ya jamii. Mawasiliano ni njia inayofanya kazi kama daraja kati ya watu au jamii mbili zinazotumia lugha tofauti. Mfano maelekezo ya insi ya kutumia bidhaa kama vile dawa, simu redio n.k, pia mikataba ya kimataifa hutafsiriwa katika lugha mbalimbali kutegemeana na jamii husika.
Karibu mataifa yote yanatambua umuhimu wa jamii ya kimataifa. Nayo jamii ya kimataifa imeafikiana maazimio mengi kuhusu tabia, hali na mienendo ya watu, kama vile haki za kibinadamu, haki za watoto na umuhimu wa mazingara ya ulimwengu. Maazimio haya yametafsiriwa kwa lugha zinazozungumzwa kwa wingi ili kufikia watu wengi iwezekanavyo. Watawala wa mataifa binafsi nao wanahakikisha kuwa taarifa muhimu kwa jamii yote zimetafsiri kwa lugha inayoeleweka na raia wengi, ili waweze kujisomea au kusomewa na wenzao. Humu nchini makala nyingi ambazo hapo awali zilikuwa zimeandikwa kwa Kiingereza zimefatafsiriwa au kufanyiwa mpango wa kutafsiriwa kwa Kiswahili.

Utamaduni unahusu maswala mengi ya maisha ya jamii. Hapa tutafikiria zaidi falsafa za maisha, zinavyoenezwa kupitia matumizi ya lugha na fasihi. Ngano na tanzu zingine za fasihi ni hifadhi za tamaduni za lugha zake. Tunapotafsiri fasihi, tunafuma baadhi ya vipengele vya utamaduni wa lugha chasili kwa utamaduni wa lugha pokezi. Mafunzo yanayopatikana katika tafsiri za lugha zingine za Kiafrika -fasihi simulizi– sasa ni amali ya Kiswahili. Tafsiri za Kiarabu, Kiingereza na lugha zingine pia zimechangia ujenzi wa lugha ya Kiswahili. Tunapotafsiri pia tunajenga lugha pokezi: lugha pokezi inamotishwa kukua na wakati wake na kumiliki nyenzo za kuhimili miradi ya kijamii.  Mfano 

Dini ni nguzo muhimu inayohimili jamii nyingi. Katika kusambaza utamaduni na Imani za Kikristo, wamishenari walitafsiri Biblia na mafunzo mengine kwa lugha nyingi kote ulimwenguni.  Vilevile, Waislami walitumia mbinu kama hiyo  na  kutafsiri  Korani na mafunzo kama Hadithi kwa lugha nyingi. Ni jambo rahisi zaidi kufikia roho ya mtu kwa lugha yake kuliko ile ya wageni. Bila tafsiri, dini nyingi hazingesambaa kadiri zimekuja kufanikiwa. Kumbuka, dini hizi zilisambaa sawia elimu ya mwegemeo wake.
Mbinu ya kujifunza lugha za kigeni, mfasiri anapofanya kazi ya kutafsiri hukumbana na changamoto mbalimbali na anapohitaji kuzitatua changamoto hizo hujifunza lugha katika kipengele cha msamiati, sarufi, maana na nyongeza au maana za kimuktadha.

UAINISHAJI WA MATINI ZA TAFSIRI

Kuainisha matini ni kuzigawa au kuziweka matini katika makundi mbalimbali kwa kuzingatia kufanana kwake kwa sifa kadhaa.
Sababu za kuainisha matini za tafsiri, Ili kupata aina au makundi kadhaa yatakayotuongoza kuchagua njia au mbinu ya kutafsiri. Hii ni kwa sababu kila aina fulani ya matini hutafsiriwa vizuri zaidi kwa kutumia njia au mbinu fulani.
Mikabala /vigezo vya uainishaji wa matini za tafsiri
a)      Kigezo cha mada
b)      Matumizi ya istilahi
c)      Dhima kuu za lugha

a)      Kigezo cha mada/maudhui

Katika kigezo hiki kinachoangaliwa ni kwamba matini inaongelea nini au inahusu nini kwa mtazamo wa kijumla. Kwa kutumia kigezo hiki cha mada tunapata aina tatu za matini;
        i.            Matini za kifasihi. Ni matini zinazohusu maandiko ya kifasihi kama hadithi fupi, riwaya, tamthiliya, ushairi n.k.
      ii.            Matini za kiasasi.  Ni matini zinazohusu siasa, biashara, fedha, sheria, serikali na asasi nyinginezo. Mfano wa Matini hizi za kimamlaka ni kama vile matini za
kisiasa na kiserikali (hotuba, risala, mikataba, vyeti nk).
    iii.            Matini za kisayansi. Ni matini zinazojumuisha nyanja zote za sayansi na teknolojia. Mfano maelekezo ya matumizi ya vifaa mbalimbali vya kielektroniki

b)     Kigezo cha matumizi ya istilahi

Kigezo hiki huangalia kiwango cha matumizi ya istilahi za uwanja fulani hivyo matini huainishwa kwa kuangalia wingi au idadi za istilahi au msamiati maalumu kwa ajili ya taaluma husika. Hivyo kwa kuangalia idadi ya istilahi tunapata aina tatu za tafsiri ambazo ni; 
                                            i.            Kiufundi
                                          ii.            Nusu-ufundi
                                        iii.            Matini zisizo za kiufundi (matini za kawaida)
i)                   Matini za kiufundi (Technical text), hizi huwa na idadi/matumizi makubwa ya istilahi.
ii)                 Matini za nusu ufundi (Semi-Techinical Text), huwa na kiwango cha kati cha matumizi ya istilahi (zinakuwa na istilahi chache).
iii)               Matini zisizo za kiufundi (Non-technical text), hizi zinakuwa hazina matumizi ya istilahi na hivyo hutumia msamiati wa kawaida

c)      Kigezo cha dhima kuu za lugha

Kwa kutumia kigezo hiki matini za tafsiri huainishwa kwa kufuata aina za dhima kuu za lugha zilizopendekezwa na Bülher (1965) ambazo ni;
    (I)            
              Dhima elezi (Expressive function);
Ni aina ya matini ambayo hujiegemeza zaidi kwa mwandishi, mwandishi anatumia lugha kuelezea hisia zake bila kujali ujumbe huo utapokelewa vipi na wasomaji. Mfano mzuri wa matini elezi ni kazi mbalimbali za fasihi kama vile: ushairi, hadithi fupi, tamthiliya, riwaya, hotuba, nyaraka za kisheria, wasifu nafsi, insha nk.
  (II)            
                Dhima   arifu (Informative function)
Hapa lugha hutumika kutolea taarifa. Kiini cha dhima hii ni ukweli wa mambo/taarifa yenyewe. Matini hizi huwa zinaandikwa katika maumbo sanifu, mfano vitabu, ripoti za kiufundi, tasnifu au Makala katika magazeti ama majarida ya kitaaluma n.k
(III)             
               Dhima amili (Persuasive function)
Ni aina ya matini ambayo imeegemea zaidi upande wa wasomaji. Matini amili zinalenga kuibua hisia za msomaji na kumfanya afikiri au atende kwa maana ambavyo imekusudiwa na matini mahususi. Hivyo lugha hutumika kuchochea hisia za msomaji na kiini cha dhima hii ni hadhira. Mfano wa matini hizi ni matangazo, maombi mathalani ya kazi au kitu kingine, maelekezo, propaganda na mialiko.
Kwa kuzingatia dhima hizo tatu za lugha kwa mujibu wa Bülher (1965) tunapata aina tatu za matini ambazo ni;
i)                   Matini Elezi
Matini hizi huegemea zaidi upande wa mwandishi, mfano fasihi, maandiko ya kimamlaka kama vile hotuba, mikataba, maandiko ya kisheria, maandiko ya kitaaluma, wasifu, tawasifu, shajara, wosia n.k.
ii)                 Matini arifu
Matini ambazo hulenga kutoa taarifa na hata maarifa kuhusu jambo fulani kama vile vitabu vya masomo/taaluma mbalimbali. Matini arifu huwa na muundo maalumu Mfano; umbo la jarida, makala, ripoti, tasnifu, vitabu vya taaluma mbalimbali n.k.
iii)               Matini amili
Matini amili huegemea zaidi upande wa hadhira, Katika matini Amili mwandishi hujitahidi kadiri awezavyo kuchochea hisia za wasomaji na kuwafanya watende kama ambavyo anavyotaka watende/wafanye. Mfano wa matini hizo ni kama vile mialiko (barua na kadi, matangazo, maelekezo (jinsi ya kutumia kitu) n.k.
 


UCHAMBUZI WA MATINI ZA TAFSIRI


Kuchambua matini maana yake ni kuisoma matini husika kwa kina na kuielewa kabla ya kuanza kuifasiri/kuitafsiri. Pia sababu au umuhimu wa kuchambua matini za tafsiri ni ili kubaini sifa na vipengele vinavyojenga matini husika kifani, kimaudhui na hata kiitikadi.



Hatua na vipengele vya uchambuzi wa matini

Kuna vipengele vikuu vitatu, ambapo kila kipengele kina hatua kadhaa ndogondogo.
             i.    Kusoma matini nzima/yote. Faida ya hatua hii ni kwamba humsaidia mfasiri kuweza kuandaa marejeleo muafaka, kuandaa vitabu au machapisho mbalimbali (kama vile kamusi ya lugha moja au mbili) yatayomsaidia katika zoezi zima la kufasiri matini. Pia hatua hii itamsaidia mfasiri kuandaa orodha ya istilahi na visawe vitakavyohitajika katika suala zima la tafsiri. Vilevile itamwezesha mfasiri kugawa vipengele/sehemu miongoni mwa wafasili hasa kama matini ni kubwa.

                ii.        Kuchambua matini yenyewe. Uchambuzi wa matini hulenga kupata nduni/sifa bainifu za matini husika. Kipengele hiki kina hatua tano kama ifuatavyo;
a)      Kubaini lengo la mwandishi wa matini chanzi. Mfano; malengo ya mwandishi huweza kuwa kukweza, kubeza kusifu, kukashfu au kuarifu jambo. Hivyo katika uandishi mwandishi anaweza kuwa na mtazamo mmoja kati ya hii mitatu;
Ø  Mtazamo hasi kwa mtendwa
Ø  Mtazamo chanya kwa mtendwa
Ø  Mtazamo wa kati.
b)      Kubaini lengo la mfasiri (mteja). Mfasiri hapa inabidi ajiulize kwa nini anataka kutafsiri matini husika. Pia mfasiri ajiulize kwa nini mteja wake anataka matini hiyo itafsiriwe. Hivyo mfasiri anapaswa kuepuka upendeleo au kuegemea upande mmoja badala yake anapaswa kuwa na msimamo wa katikati hata hivyo ni muhimu sana kwa mfasiri kuzingatia hadhira lengwa.
c)      Kubaini hadhira na umbo la matini. Hapa mfasiri atajiuliza maswali kama vile: - hiyo matini anayofasiri ni aina gani ya matini? je aina hiyo ya matini inatafsirika vizuri zaidi kwa kutumia njia/mbinu gani? Je hadira lengwa ya zao la tafsiri ni ipi na ina sifa gani? Mfano hadhira wana elimu hadi ngazi ipi, umri wao, mahali wanapoishi n.k. Pia zao la tafsiri linapaswa kuwa katika umbo gani?
d)      Kubaini mtindo wa matini. Ni muhimu sana mtindo wa matini chanzi kujitokeza katika matini lengwa. Mfano kama matini chanzi ipo kwenye mtindo wa monolojia, dailojia, hadithi, lugha za mitaani au mtindo wa kidini hivyohivyo matini lengwa inatakiwa kuwa katika mtindo wa matini chanzi.
e)      Kubaini ubora na mamlaka ya matini. Ubora wa matini chanzi hutokana na kuzingatia zana za kiisimu. Hivyo mfasiri hanabudi kuzingatia ujuzi wa mwandishi katika kutumia zana za kiisimu (vipengele mbalimbali vya lugha). Kwa upande wa mamlaka ya matini chanzi hutokana na hadhi/ubobevu wa mwandishi katika taaluma husika.
    iii.            Kusoma matini kwa mara ya mwisho. Mfasiri katika hatua hii inabidi asome tena matini chanzi ili kutoa taswira au kuwekea alama maneno au maumbo muhimu katika matini. Baadhi ya maneno au mambo huhimu ya kuzingatia ni kama vile majina mahsusi ya watu, sehemu, takwimu na pia miaka. Vilevile kuna maneno ambayo hayatafsiriki kirahisi hivyo itambidi mfasiri ayawekee alama ili iwe rahisi kwake katika kutafuta visawe.

MCHAKATO WA KUFASIRI

     Hatua muhimu za kutafsiri

Baadhi ya wataalamu wanasema kuna hatua 5 wengine 6,7 na wengine wanadai zipo hatua 8. Hapa tutchambua hatua 6 kama zinavyopendekezwa na Mwansoko na wenzake 2006.

Hatua hizo zilizoainishwa na Mwansoko na wenzake 2006 ni zifuatazo;
                              i.            Maandalizi
                              ii.            Uhawilishaji
                            iii.            Kusawidi rasimu ya kwanza ya tafsiri (drafting)
                            iv.            Kudurusu wa rasimu ya kwanza ili kupata rasimu ya pili ya tafsiri
                              v.            Kusomwa kwa rasimu ya pili na mtu mwingine
                            vi.            Kusawidi wa rasimu ya mwisho ya tafsiri


i.                    Maandalizi ya kutafsiri

Hatua hii inahusisha mambo matatu ambayo ni: 
    a)   Kupitia tena sehemu muhimu za matini chanzi, kwa mfano; istilahi, majina ya wahusika, majina ya kijiografia, maeneo au kauli zisizofasirika kirahisi.
    b)      Kupata marejeleo ili kutafuta visawe vya kisemantiki kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
     c)      Kutafuta na kuandika maneno au visawe hivyo.

Hivyo katika hatua hii, mfasiri anatakiwa kufahamu vizuri maudhui ya matini chanzi, ujumbe wake, mtindo wa matini na kuwekea alama sehemu zenye utata au zisizoeleweka vizuri, anashauriwa kupigia mstari au kuandika katika kidaftari kidogo msamiati, istilahi na misemo muhimu ya matini chanzi kama vile, methali, nahau maneno ya kitamaduni yasiyotafsirika, majina maalumu, n.k. kwa kupigia mstari au kuyaandika katika kidaftari kidogo ili iwe rahisi kwa mfasiri kuyatafutia visawe vyake kabla hata ya kuanza kutafsiri lakini pia kumsaidia mfasiri asiyasahau wakati wa kutafsiri au kuyatolea ufafanuzi zaidi katika tafsiri yake.

ii.                  Uhawilishaji

Uahawilishaji maana yake ni kuhamisha ujumbe, maana n.k kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa, lengo, mawazo, umbo la matini, mtindo wa matini n.k. Hii ina maana kuwa katika hatua hii, visawe vya kisemantiki [kimaana] vya matini chanzi vilivyobainishwa katika hatua ya awali (maandalizi) huamishwa katika matini lengwa [kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa] na kupangwa vizuri kisarufi na kimantiki ili fasiri hiyo iwe na maana kwa wasomaji wake.

iii.                Kusawidi rasimu ya kwanza ya tafsiri (drafting)

Uhawilishaji wa visawe kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa unapokamilika kinachopatikana ni rasimu ya kwanza ya tafsiri. Katika hatua hii, mfasiri huandika rasimu yake ya kwanza ili kupata picha fulani ya matini aliyoikusudia, katika uandaaji wa rasimu ya kwanza, kwa kufanya hivi, mfasiri anaweza kugundua kuwa anahitaji taarifa zaidi tofauti na alizozipata katika hatua ya awali, na hivyo kulazimika kuchunguza zaidi matini chanzi na hata kupekua zaidi na zaidi marejeo yake aliyoyaandaa kwa kuyatumia katika tafsiri. Jambo la kuzingatia, mfasiri anatakiwa wakati akihamisha mawazo au ujumbe azingatie umbo na lengo la matini chanzi ili kutoathiri tafsiri yake. Hivyo rasimu ya kwanza ya tafsiri inakuwa na dosari nyingi na kwa hiyo haifai kupelekwa kwa mteja au hadhira. Badala yake rasimu ya kwanza lazima ipitiwe tena upya na kurekebishwa au kudurusiwa/durusu (review) rasimu (draft).

iv.                Kudurusu rasimu ya kwanza ili kupata rasimu ya pili

Baada ya kusawidi rasimu ya kwanza, mfasiri anatakiwa kuivundika rasimu yake ya tafsiri, Larson (1984) anashauri kuwa rasimu ya kwanza iachwe kwa muda kidogo kati ya juma moja hadi mawili tangu kukamilika kwake na kuanza kuidurusu/ kuipitia rasimu hiyo kwa jicho la kihakiki zaidi na kuangalia kama kuna makosa ambayo yamejitokeza katika rasimu yake au la na kuyafanyia marekebisho pale inapobidi. Mfasiri katika hatua hii anatakiwa kuisoma rasimu yote ya tafsiri (kwa sauti) ili aweze kufanya mambo yafuatayo;
ð  Kunyoosha sehemu zenye tafsiri ya mzunguko na zenye matumizi potofu ya visawe.
ð  Kurekebisha sehemu zenye miunganiko tenge inayozuia mtiririko mzuri wa matini.
ð  Kuhakiki usahihi na ukubalifu wa maana zilizowasilishwa katika matini lengwa.
ð  Kuhakiki ukubalifu wa lugha iliyotumika katika matini lengwa kulingana na umbo la matini ya lugha chanzi.
ð  Kuona iwapo mada au ujumbe mkuu wa matini chanzi unajitokeza waziwazi katika matini lengwa.

v.                  Kusomwa rasimu ya pili na mtu mwingine

Matokeo ya kudurusu rasimu ya kwanza huwa ni kupatikana kwa rasimu ya pili. Ingawa rasimu ya pili inakuwa bora zaidi kuliko rasimu ya kwanza bado kuna haja ya ya rasimu ya pili kusomwa na mtu mwingine tofauti na mfasiri mwenyewe. Hii ni kwa sababu mtu wa pili anaweza kung’amua dosari ambazo mfasiri hakuziona. Msomaji wa pili anaweza kuwa mfasiri, shabiki wa tafsiri, mhakiki wa tafsiri, mhariri, mteja wako au mtu mwingine unayemwamini.
Pia wakati mwingine msomaji wa pili hatakiwi kujua kwamba anachosoma ni tafsiri hivyo mfasiri anaweza kumficha. Hivyo ni vizuri zaidi msomaji wa pili kusoma kwa sauti ili aone ni wapi hapana mtiririko mzuri (yaani wapi anakwamakwama) ili aweke alama ambapo anakwama ili kumsaidia mfasiri wakati wa kurekebisha.

 

vi.                Kusawidi rasimu ya mwisho

Katika hatua hii mfasiri atafanyia kazi maoni ya msomaji wa pili, mfasiri anaweza kuyatumia maoni, mapendekezo na maelekezo ya msomaji wa pili akiona yanafaa ili kuweza kusahihisha tafsiri yake na hatimaye kuandaa na kutoa rasimu ya mwisho ambayo kwa hakika ndiyo tafsiri yenyewe iliyokamilika. Rasimu hii ya mwisho ndiyo hupelekwa kwa mteja, hadhira, au wachapaji (kuchapisha kuwa kitabu) iwapo hilo ndilo lengo.

AINA NA MBINU/NJIA ZA KUTAFSIRI


 
TAFSIRI NA UKALIMANI.Pdf

UKALIMANI


Dhana ya ukalimani

Kwa mujibu wa KADE (1968) anafasili ukalimani kuwa ni aina fulani ya tafsiri ambapo matinichanzi huwasilishwa mara moja pekee na hivyo haiwezi kupitiwa upya, kuchezwa upya au kurudiwa pia matini lengwa hutolewa katika muda finyu huku kukiwa hakuna fursa ya marudio au masahihisho na kama fursa hiyo ipo basi ni finyu sana.
Naye Pӧchhacker (2004) aliboresha fasili iliyotolewa na KADE (1968) na kuja na fasili ifuatayo ya ukalimani, anasema ukalimani ni aina fulani ya tafsiri ambapo matini lengwa hutolewa mara moja tu katika muda finyu na kwa ajili ya matumizi ya muda wa wakati huohuo.
Hivyo basi kwa kuangalia fasili hizo mbili tunaweza baini kuwa msingi wa ukalimani ni hali ya papo kwa papo ya uwasilishaji.
Kwa jumla, ukalimani ni uhawilishaji wa ujumbe au maudhui yaliyo katika matini chanzi kwenda katika lugha lengwa ambapo mkalimani hubanwa na muda na hivyo kukosa fursa ya kurudia kusikia matini chanzi wala kuihawilisha lakini pia uhawilishaji hulenga kuinufaisha hadhira lengwa papo hapo.

Sifa za Mkalimani

      a)      Awe na ujuzi wa hali ya juu wa lugha anazoshughulika nazo pamoja na utamaduni wake.
      b)      Ajue lugha zaidi ya mbili za kimataifa kwani kadiri unavyojua lugha zaidi ndivyo unavyokuwa   mkalimani bora zaidi. Pia lugha zaidi ya moja hasa za kimataifa zitamsaidia sana hasa kwenye mikutano/makongamano.
     c)      Awe na ujuzi au maarifa ya kutosha juu ya mada, taaluma au uwanja unaozungumziwa. Inamaana kwamba kama wewe ni mkalimani wa masuala ya kiuchumi basi hupaswi kufasili masuala ya kisheria. Mfano; ukalimani wa mahakamani hufanywa na wanasheria, masuala ya tiba n.k
    d)      Awe na ujuzi wa taaluma ya ukalimani; yaani awe amepata mafunzo ya ukalimani. Katika hayo mafunzo atajifunza mbinu za ukalimani aina, changamoto na namna ya kuzikabili changamoto hizo.
     e)      Awe na kipaji, yaani; Yaani uwezo wa kukumbuka kwa hali ya juu, Kuteua msamiati sahihi kwa haraka, Kipaji katika kuunda istilahi haraka haraka na kuitumia. Kipaji cha ulumbi/awe na ulumbi yaani kipaji cha kuongea na kuvuta/kushawishi watu.
    f)  Awe mchapakazi, mdadisi na nayependa kujiendeleza na kupata  habari kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii mfano; magazeti, majarida, televisheni, facebook, twitter au kuzungumza na watu/kuchangamana na watu.
J     
                 
TAFSIRI NA UKLIMANI.Pdf



TFSIRI NA UKALIMANI
J
 



Pata kitini cha tafsiri na ukalimani bure kabisa. Kitini hiki kimejaribu kuchambua tafsiri na ukalimani kwa ajili ya kuwapa mwanga wanafunzi wa ngazi zote kuanzia shule za sekondari hadi chuo kikuu. 

Pia kitini hiki kimeandikwa kwa kurejelea wataalamu mbalimbali ambao ni mashuhuri sana katika suala zima la Tafsiri na Ukalimani.


📜  Pia Notes zote na past papers za i-iv     unaweza kuzipata kupitia hapa📚



COMMENTS

BLOGGER
Name

Afya,4,Ajira,2657,Audio,26,Biashara,2,Burudani,43,Economics,1,ELIMU,26,Gossip,38,Habari,2861,History,2,Kimataifa,202,kisiasa,13,Kiswahili,6,Kitaifa,147,Magazeti,44,Matokeo,3,Matukio,89,Michezo,2829,Muziki,62,Nairobi aiport,1,Ripoti,4,Tools,1,Video,47,Vituko,15,
ltr
item
Antagon Blog: TAFSIRI NA UKALIMANI
TAFSIRI NA UKALIMANI
Tafsiri na ukalimani
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEijwkJuX7jUMxyZxME3eIv29n7GGs1EhocyAmIn6Ax6zaS13dp753iXQU6ioK7sN-IEH9B87eUjXJkfnpp9ZisIomYMtOEq_CA6aIEuLasnfGumjmZWiNv48yPR6u0GyM_dEkP5BL8bPdCA/s640/images.jpg
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEijwkJuX7jUMxyZxME3eIv29n7GGs1EhocyAmIn6Ax6zaS13dp753iXQU6ioK7sN-IEH9B87eUjXJkfnpp9ZisIomYMtOEq_CA6aIEuLasnfGumjmZWiNv48yPR6u0GyM_dEkP5BL8bPdCA/s72-c/images.jpg
Antagon Blog
http://antagonf.blogspot.com/2014/10/tafsiri-na-ukalimani.html
http://antagonf.blogspot.com/
http://antagonf.blogspot.com/
http://antagonf.blogspot.com/2014/10/tafsiri-na-ukalimani.html
true
8268252095325502418
UTF-8
Loaded All Posts Not found any posts VIEW ALL Readmore Reply Cancel reply Delete By Home PAGES POSTS View All RECOMMENDED FOR YOU LABEL ARCHIVE SEARCH ALL POSTS Not found any post match with your request Back Home Sunday Monday Tuesday Wednesday Thursday Friday Saturday Sun Mon Tue Wed Thu Fri Sat January February March April May June July August September October November December Jan Feb Mar Apr May Jun Jul Aug Sep Oct Nov Dec just now 1 minute ago $$1$$ minutes ago 1 hour ago $$1$$ hours ago Yesterday $$1$$ days ago $$1$$ weeks ago more than 5 weeks ago Followers Follow THIS CONTENT IS PREMIUM Please share to unlock Copy All Code Select All Code All codes were copied to your clipboard Can not copy the codes / texts, please press [CTRL]+[C] (or CMD+C with Mac) to copy